Storm FM

Marufuku watoto kwenye Mabanda ya video Geita Road

29 August 2025, 5:16 pm

Picha hii kutoka mtandaoni ikionesha baadhi ya watoto wakiwa katika banda la video. Picha na Mtandao

Sera ya maendeleo ya mtoto ya mwaka 2008 inaweka bayana wajibu wa jamii, wazazi na serikali kulinda watoto dhidi ya vitendo vinavyoweza kuathiri makuzi yao.

Na Mwandishi Wetu:

Mwenyekiti wa mtaa huo Pelana Bagume amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kuongezeka kwa malalamiko ya watoto wengi kuacha kuhudhuria masomo shuleni na badala yake kutumia muda mwingi kwenye vibanda hivyo, jambo linalohatarisha elimu na maadili yao.

Bagume amesisitiza kuwa serikali ya mtaa itachukua hatua za kisheria kwa mmiliki yeyote wa kibanda atakayebainika kuruhusu watoto kuingia, kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009, ambayo inakataza mtoto kushiriki shughuli zinazoweza kuhatarisha afya, maendeleo na maadili yake.

Aidha, hatua hiyo pia inakwenda sambamba na Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008, ambayo inaweka bayana wajibu wa jamii, wazazi na serikali kulinda watoto dhidi ya vitendo vinavyoweza kuathiri makuzi yao, pamoja na kuhakikisha wanalindwa dhidi ya maudhui hatarishi yanayopatikana kwenye vyombo vya habari na burudani.

Kwa upande wao, baadhi ya wamiliki wa vibanda vya video wameahidi kushirikiana na serikali kwa kuhakikisha wanadhibiti mienendo ya watoto, huku wakiahidi kuweka matangazo ya wazi ya kuzuia watoto kuingia.

Nao baadhi ya wazazi na walezi wamesema wako tayari kushirikiana na uongozi wa mtaa kwa kufuatilia mienendo ya watoto wao, huku wakikiri kuwa teknolojia na vyanzo visivyo rasmi vya burudani vimekuwa kikwazo katika malezi bora.

Wadau wa elimu na ulinzi wa mtoto katika eneo hilo wamesisitiza kuwa utekelezaji wa sheria na sera hizo ni muhimu ili kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama, wakisisitiza kuwa malezi bora ndiyo msingi wa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Ripoti ya stori hii na Mrisho Sadick