Storm FM

Sakata la TFS na wananchi Lwamgasa limekwisha

20 August 2025, 8:21 pm

Mamia ya wakazi wa Rwamgasa wakiwa kwenye mkutano wa kutafuta suluhu ya mgogoro na TFS. Picha na Mrisho Sadick

Miongoni mwa sababu kubwa za mgogoro huu ni uhaba wa maeneo ya kilimo, hali inayochangiwa na shughuli nyingi za uchimbaji wa madini ya dhahabu.

Na Mrisho Sadick:

Siku chache baada ya wakazi wa kijiji cha Lwamgasa wilayani Geita kuvamia na kuivunja Ofisi ya TFS kisha kuwashambulia askari wanne wa TFS , kuchoma moto shamba la miti, Baiskeli na Pikipiki kwa madai ya kuzuiwa kufanya shughuli za kilimo katika eneo hilo, serikali kwa kushirikiana na TFS hatimaye imetafuta suluhu kwa kuwaruhusu wananchi kulima huku taratibu nyingine zikiendelea.

Katika jitihada za kupata maridhiano, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Geita ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Hashim Komba, maafisa wa TFS kutoka Kanda na Makao Makuu pamoja na viongozi mbalimbali wamekutana na mamia ya wananchi wa kijiji cha Lwamgasa Katika mkutano huo wananchi wameeleza kwa uchungu kero zao za kutokuwa na ardhi ya kutosha kwa kilimo.

Mkuu wa wilaya ya Geita akiwa kwenye mkutano wa kutafuta suluhu ya wananchi na TFS Rwamgasa. Picha na Mrisho Sadick

Miongoni mwa sababu kubwa za mgogoro huu ni uhaba wa maeneo ya kilimo, hali inayochangiwa na shughuli nyingi za uchimbaji wa madini ya dhahabu katika kijiji hicho hiki huku Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba akiwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi pindi wanapohitaji jambo na  akatoa msimamo wa serikali kuhusu madai ya wananchi.

Aidha, DC Komba amesisitiza kuwa lazima kuwepo na mahusiano mazuri kati ya wananchi na TFS, akionya kuwa migogoro kama hii isijirudie tena nakwamba watu waliotekeleza kitendo hicho hawatavumiliwa.

Baada ya kauli hiyo ya serikali wananchi hawakusita kuonesha hisia zao kwa kupongeza hatua hiyo, wengine wakieleza kuwa angalau sasa wamepata mwanga wa matumaini ya kujikimu kupitia kilimo.

Viongozi mbalimbali na maafisa wa TFS wakiwa kwenye mkutano wa kutafuta utatuzi wa mgogoro. Picha na Mrisho Sadick

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita kwa upande wake lilieleza kuwa limewakamata watu 50 waliodaiwa kuhusika na uharibifu wa ofisi, kuchoma moto shamba na mali za TFS hata hivyo 40 kati yao wameachiwa huru huku 10 wakiendelea kushikiliwa kwa mahojiano ili kubaini wahusika wakuu wa tukio hilo.

Sauti ya ripoti ya stori hii