Storm FM

Milioni 60 zahitajika jengo la mama na mtoto Chato

19 August 2025, 4:04 pm

Jengo la mama na mtoto linalohitaji ukamilishaji Buseresere wilayani Chato. Picha na Mrisho Sadick

Hadi sasa tayari shilingi milioni 3 zimekusanywa kupitia jitihada za jamii na wadau mbalimbali, kati ya milioni 60 zinazohitajika

Na Mrisho Sadick:

Zahanati ya Buseresere Wilayani Chato inahitaji jumla ya shilingi milioni 60 ili kukamilisha ujenzi wa jengo la mama na mtoto lililodumu kwa zaidi ya miaka 14 bila kufanyiwa ukamilishaji.

Akizungumza katika mbio za hisani zilizolenga kuchangia ukamilishaji wa jengo hilo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Chato Thomas Dime amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri kutenga fedha kupitia mapato ya ndani ili kuhakikisha ndoto ya wananchi wa eneo hilo inatimia.

Sauti ya katibu tawala Chato
Katibu tawala wilaya ya Chato Thomas Dime akizungumza kwenye mbio za hisani za kuchangia ukamilishaji Jengo la mama na mtoto. Picha na Mrisho Sadick

Mratibu wa huduma za afya ya uzazi na mtoto, Ezron Yuda, pamoja na Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Buseresere, Edmundi Wilbad, wamesema wameanzisha mbio za hisani zilizojulikana kama Tuwavushe Mama na Mtoto Buseresere Marathonili kusaidia kufanikisha ujenzi huo na kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto.

Sauti ya Mratibu wa afya na Mfawidhi Buseresere
Baadhi ya washiriki wa mbio za hisani wilayani Chato za kuchangia ujenzi wa jengo la mama na mtoto. Picha na Mrisho Sadick

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Dkt. Daniel Mzee amesema kutokana na udogo wa miundombinu ya zahanati hiyo, serikali imepanua huduma katika maeneo jirani ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mapinduzi ili kupunguza msongamano wa wagonjwa.

Sauti ya Mganga Mkuu Chato