Storm FM
Storm FM
15 August 2025, 5:34 pm

Upungufu wa maeneo ya shughuli za kibinadamu kama kilimo imekuwa sababu ya kuongezeka kwa matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi na kuvamia maeneo ya hifadhi.
Na Mrisho Sadick:
Wananchi wa kitongoji cha CCM kijiji cha Lwamgasa wilaya ya Geita mkoani Geita wameteketeza kwa moto hifadhi ya shamba la Miti la Lwamgasa na kuharibu ofisi ya wakala wa huduma za misitu Tanzania TFS kwa madai ya kukerwa na manyanyaso ya askari wa hifadhi hiyo ikiwemo kuzuiwa kufanya shughuli za kilimo.
Tukio hili limetokea Agosti 13, 2025 majira ya saa 7 mchana, ndani ya hifadhi hiyo baada ya kundi la wananchi wakazi wa Kijiji cha Lwamgasa kuvamia ofisi hiyo nakufanya uharibifu wa Jengo na nyaraka mbalimbali zilizokuwa ndani ya Ofisi hiyo kisha kuchoma moto Shamba la miti katika eneo hilo.

Mwenyekiti wa kitongoji cha CCMÂ Bahati Charles amedai kuwa amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kushambuliwa na askari na TFS katika eneo hilo ndio sababu ya wao kuchukua hatua ya kufanya uharibifu huo.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Geita ACP Adam Maro amesema kutokana na tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linawashikilia watuhumiwa hamsini (50) kwa tuhuma za kuvamia Ofisi hiyo ,kuwashambulia na kuwajeruhi Maafisa wa Misitu wanne (4) na kuharibu mali mbalimbali za ofisi ikiwemo kuchoma moto pikipiki moja na miche ya miti 50,000 iliyokuwa kwenye vitalu imeandaliwa kupandwa na miti 236,643 ambayo tayari ilikuwa imepandwa.

Amesema chanzo cha tukio hili ni kundi la wananchi hao kujichukulia sheria mkononi kwa kuwazuia Maafisa hao wasitekeleze majukumu yao, Jeshi la Polisi linaendelea kuwahoji watuhumiwa hao na upelelezi utakapokamilika watafikishwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa wananchi wote kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mkononi na halitasita kuchukua hatua kali za kisheria, badala yake linawataka wananchi kutumia njia sahihi za kuwasilisha madai yao kwenye mamlaka zinazohusika.