Storm FM
Storm FM
11 August 2025, 1:09 pm

Mashindano hayo ni zaidi ya burudani kwani yanatoa nafasi kwa vijana kuonesha vipaji ambavyo havijaonekana kitaifa.
Na Mwandishi Wetu:
Mwamuzi maarufu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Ally Simba ameonesha kuridhishwa na kiwango cha ushindani na nidhamu ya wachezaji katika michuano ya Mapung’o Cup inayoendelea kutimua vumbi mkoani Geita huku akizitaka taasisi mbalimbali zinazosaka vipaji kutembelea eneo hilo kwani huenda wakapata vijana wengi.
Akizungumza baada ya mchezo wa robo fainali kati ya Nyasubi FC na Bugarama FC kumalizika Simba ameeleza kuwa mashindano hayo ni zaidi ya burudani kwani yanatoa nafasi kwa vijana kuonesha vipaji ambavyo havijaonekana kitaifa nakwamba michuano hiyo imejipatia heshima tangu kuanzishwa kwake kwa kuibua wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kucheza soka la ushindani.

Katika mwendelezo wa michuano hiyo timu ya Nyasubi FC kutoka Kahama imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Mapung’o Cup 2025 baada ya kuifunga Bugarama FC bao 1- 0,bao hilo pekee limeifanya Nyasubi FC kufuzu kwa jumla ya mabao 2-0, baada ya pia kushinda mechi ya kwanza ya robo fainali.

Kocha wa Nyasubi FC, Elisha Emmanuel, amesema timu yake ina morali na ari kubwa, na lengo lao ni kuhakikisha wanatinga hatua ya fainali nakuchukua ubingwa huku kocha wa Bugarama FC akitokomea kusikojulikana baada ya kupoteza mchezo huo.
Mashindano ya Mapung’o Cup yanashirikisha timu kutoka mikoa mbalimbali ya Kanda ya Ziwa na yana dhaminiwa na mdau maarufu wa soka Pascal Mapung’o anayefahamika kama King Mapung’o.