Storm FM

Karakana nyingine yateketea kwa moto Geita

4 August 2025, 4:13 pm

Sehemu ya Karakana iliyoteketea kwa moto alfajiri ya leo Mtaa wa Mkoani . Picha na Kale Chongela

Matukio ya moto kuteketeza karakana yameendelea kuongezeka mkoani Geita huku sababu za matukio hayo zikiwa hazijulikani.

Na Kale Chongela:

Moto mkubwa ambao chanzo chake bado hakijajulikana umeteketeza karakana moja ya useremala katika mtaa wa Mkoani, Kata ya Kalangalala, Manispaa ya Geita Mkoani Geita na kusababisha hasara inayokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi milioni 10.

Tukio hilo limetokea alfajiri ya leo Agosti 04,2025  na limeacha simanzi kubwa kwa mmiliki wa karakana hiyo kutokana na kuungua kwa samani na vifaa vyote vya kazi vilivyokuwemo ndani.

Hili ni tukio la pili la aina hii kutokea ndani ya kipindi cha wiki moja katika Kata hiyo ambapo karakana nyingine iliteketea kwa moto katika mtaa wa Nyerere na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.

Sehemu ya Karakana iliyoteketea kwa moto alfajiri ya leo Mtaa wa Mkoani . Picha na Kale Chongela

Baadhi ya majirani na mashuhuda wa tukio hilo waliopambana na moto huo kwa kutumia vifaa vya kawaida ili kuzuia usienee kwenye makazi yao na maeneo ya biashara Edda Phinias na Marko Manda wamesema walilazimika kushirikiana kwa hali na mali kabla ya kikosi cha zimamoto kufika.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita akizungumzia tukio la moto. Picha na Kale Chongela

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Mrakibu Mwandamizi Hamisi Shabani Dawa, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo ameeleza kuwa lilitokea majira ya saa kumi na mbili alfajiri ya tarehe 4 Agosti 2025, na kwamba uchunguzi wa chanzo cha moto huo bado unaendelea.

Sauti ya Ripoti ya stori hii na Mrisho Sadick