Storm FM

GGML yatoa taulo za kike zaidi ya elfu 80 Geita

31 July 2025, 6:52 pm

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyakabale Manispaa ya Geita wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupokea taulo za kike. Picha na Ester Mabula

“Imekuwa ni desturi yetu GGML kila mwaka kuikumbuka jamii hususani kupitia masomo kwa mtoto wa kike kwa kushirikiana na serikali ya mkoa wa Geita” – Doreen kutoka GGML

Na: Ester Mabula

Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Geita Gold Minning Limited (GGML) imeendeleza mpango wa kuwasaidia watoto wa kike kuondokana na changamoto pindi wawapo kwenye hedhi kupitia mpango wa utoaji taulo za kike kwa shule za msingi na sekondari mkoani Geita.

Sambamba na hilo pia GGML imetoa elimu ya afya ya uzazi kwa walimu wa malezi wapatao 129 kutoka halmashauri ya manispaa ya Geita na halmashauri ya wilaya ya Geita kwa lengo la kuwezesha uelewa wa pamoja juu ya hedhi salama.

Katika picha ni walimu wa malezi kutoka shule za wilaya ya Geita wakiwa katika mafunzo. Picha na Ester Mabula

Wakizungumza baadhi ya walimu waliopewa mafunzo hayo leo Julai 31, 2025 afisa elimu kata ya Bugulula Mwl. Samike Deus Samike na Mwl. Rehema Mustapha ambaye ni Kaimu afisa elimu secondari halmashauri ya wilaya ya Geita wamepongeza hatua hiyo huku wakieleza imesaidia kupunguza utoro kwa watoto wa kike pindi wawapo kwenye hedhi na kwamba elimu hiyo itasaidia kuongeza motisha zaidi.

Sauti ya Mwl. Samike D. Samike na Rehema Mustapha

Wakizungumza mara baada ya zoezi la ugawaji wa taulo za kike kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari Nyakabale, mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nyakabale Bi. Veronica Samo na mwalimu wa malezi wa shule ya sekondari Nyakabale Bi. Rosemary Nichoraus wamepongeza hatua hiyo na kueleza imekuwa muarobaini katika kuongeza mahudhurio ya wanafunzi wa kike

Sauti ya Mwl. Veronica Samo na Rosemary Nichoraus
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyakabale Manispaa ya Geita wakiwa katika zoezi la kupokea taulo za kike. Picha na Mrisho Sadick

Bi. Doreen Denis kutoka idara ya uhusiano GGML amesema mgodi huo umeendelea kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya Jamii zinazouzunguka mgodi huku akieleza kuwa wametenga taulo za kike ziaidi ya elfu 80 kwaajili ya kuwasaidia watoto wa kike kwa shule 57 za mkoa wa Geita.

Sauti ya Doreen Denis kutoka GGML

Baadhi ya wanafunzi waliopewa taulo za kike wametoa pongezi kwa ggml kwa kuwapataia taulo za kike sambamba na kufadhili elimu ya Afya ya uzazi ambayo imekuwa ikiwasaidia pindi wawapo katika hedhi

Sauti ya wanafunzi

Ikumbukwe huu ni mwendelezo wa kampuni ya GGML kuendelea kuwasaidia wanafunzi wa kike ambapo hutoa taulo za kike kila mwaka.