Storm FM

Wananchi wafunguka ujenzi stendi mpya Geita

8 June 2025, 2:57 pm

Mwaka jana 2024 kituo cha mabasi Geita kilipokumbwa na mafuriko kutokana na uduni wa miundombinu. Picha na Mrisho Sadick

Baada ya kusota kwa miaka mingi hatimaye wakazi wa Geita mjini wanakwenda kupata stendi mpya ya kisasa ya mabasi.

Na Mrisho Sadick:

Watumiaji wa kituo kikuu cha mabasi ya abiria Mkoa wa Geita wameishukuru serikali kwa kutoa fedha kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 19 kwa ajili ya ujenzi wa kituo kipya cha kisasa ili kuondokana na adha wanayoipata kwasasa nyakati za mvua na jua.

Wakizungumza na Storm FM leo Juni 08,2025 katika kituo cha mabasi kinachotumika kwasasa Mwenyekiti wa kituo hicho Khalid Fereji na baadhi ya wakazi wa Geita mjini James Bunuma na Paul Shukuru wamesema wamekuwa wakipata masaibu kutokana na uduni wa miundombinu kwenye kituo hicho ambapo wameishukuru serikali baada ya Halmashauri ya Manispaa ya Geita kusaini mkataba wenye thamani ya zaidi ya bilioni 19.17 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi cha kisasa katika eneo la Magogo.

Sauti ya wananchi Geita
Muonekano wa kituo cha mabasi ya abiria cha Mkoa wa Geita asubuhi ya Juni 08,2025.Picha na Mrisho Sadick

Mwaka jana 2024 kituo hicho kilikumbwa na mafuriko hali iliyositisha shughuli kwa muda huku wananchi akiwemo Rehema Ally na Juma Juma wakitoa kilio chao kwa serikali kutoka moyoni kuonesha kuchoshwa na hali hiyo , huku vikao mbalimbali vikifanyika kukabiliana na hali hiyo.

Sauti ya wahanga wa mafuriko katika kituo cha mabasi Geita mwaka 2024

Mkandarasi wa Kampuni ya SIHOTECH Mhandisi Adam Sebastian amesema Mkataba wa ujenzi wa Kituo hicho utakuwa wa miezi 15 kuanzia juni 20 mwaka huu chini ya mkandarasi M/s SIHOTECH Engeneering Company Ltd in pamoja na AMJ Global Contractors Company Ltd huku Mkurugenzi mtendaji wa manispaa ya Geita Yefred Myenzi akiwatoa hofu wakazi wa Geita kuwa stendi hiyo itakamilika kwa wakati.

Sauti ya Mkandarasi na Mkurugenzi

Mkuu wa wilaya ya Geita Hashim Komba amesema Fedha za mradi wa kituo hicho ni sehemu ya Mkopo wa Benki ya Dunia (WB) wenye lengo la kutekeleza Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) huku mbunge wa Jimbo la Geita mjini Costantine Kanyasu akisema Kituo hicho amekipigania kwa muda mrefu nakwamba kinajengwa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 10.9 na itakuwa na uwezo wa maegesho ya mabasi 42, bajaji 100 na pikipiki 152.

Sauti ya Mbunge na Mkuu wawilaya ya Geita