Storm FM
Storm FM
27 May 2025, 2:41 pm

Jumla ya mifuko 538 ya saruji imetolewa katika ya mifuko 1,071 iliyoahidiwa ili kuweza kukamilisha ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Afya, elimu na miundombinu.
Na: Ester Mabula:
Mkuu wa wilaya ya Geita Mhe. Hashim Abdallah Komba leo Mei 27, 2025 amekabidhi mifuko 538 ya saruji kwa viongozi wa vijiji na kata zilizopo halmashauri ya wilaya ya Geita, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa kukamilika kwa wakati.
Mifuko hiyo imetolewa na Ofisi yake kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na baadhi ya viongozi wa kata na halmashauri kufuatia zaira yake mwanzoni mwa mwaka huu alipotembelea maeneo mbalimbali ya halmashauri ya wilaya ya Geita ili kusikiliza kero za wananchi pamoja na ukaguzi wa miradi ya maendeleo ambapo alibaini baadhi ya miradi iliyoibuliwa na wananchi kutokamilika kutokana na changamoto za vifaa na rasilimali.

Katika hatua nyingine, DC Komba amesema kuanzia mwezi Juni watafanya kikao maalumu na wawekezaji wanaomiliki leseni katika maeneo mbalimbali ndani ya halmashauri ili washiriki kukamilisha miradi kupitia CSR ili kuchochea zaidi maendeleo.
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Geita Dkt. Aphonce Paschal ameahidi kuwa saruji iliyotolewa itatekeleza majukumu kusudiwa na si vinginevyo.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa vijiji na kata waliokabidhiwa saruji, Diwani wa kata ya Bukoli Faraji Seif ametoa rai kwa watumishi wa serikali kutouza vifaa vinavyotolewa na badala yake vitekeleze majukumu yanayotakiwa.
