Storm FM
Storm FM
14 May 2025, 8:58 am

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Geita ikishirikiana na GGML wafungua warsha ya siku 2 kwa lengo la kutoa elimu juu ya kukabiliana na Rushwa.
Na: Ester Mabula:
Warsha hiyo, iliyoanza jana Mei 13, itaendelea leo Mei 14, 2025 katika ukumbi wa St. Aloysious mjini Geita imewakutanisha washiriki kutoka sekta mbalimbali zikiwemo taasisi za serikali, mashirika binafsi pamoja na viongozi wa jamii.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya uchimbaji Dhahabu ya Geita (GGML) Duran Achery amesema kuwa kampuni hiyo imejikita si tu katika shughuli za uchimbaji wa madini, bali pia katika kujenga jamii inayoheshimu maadili na kupinga vitendo vya rushwa.

Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Geita James Ruge amesema lengo kuu la TAKUKURU ni kudhibiti Rushwa na kusisitiza kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kama GGML ili kufanikisha azma hiyo.

Katibu tawala mkoa wa Geita Mhe. Mohamed Gombati aliyekuwa mgeni rasmi katika warsha hiyo amesema jukumu la kupambana na Rushwa ni la wote na si TAKUKURU pekee na kueleza kuwa Jamii kwa ujumla inapaswa kushiriki katika mapambano ya Rushwa.
Warsha hiyo imejumuisha mada mbalimbali zikiwemo aina za rushwa, athari zake kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, pamoja na mbinu za kuripoti vitendo vya rushwa kwa usalama na ufanisi.
Kauli mbiu ya warsha ya mwaka huu ni “Kuzuia Rushwa ni Jukumu langu na lako– Tutimize Wajibu Wetu”
Katika kampeni ya mwaka huu mbali na warsha hii ya siku mbili, pia itafanyika mikutano 28 ngazi ya vijiji ili kuhakikisha ujumbe unawafikia watu wa makundi yote katika jamii.