Storm FM
Storm FM
17 April 2025, 10:49 am

April 16, 2025 mkoa wa Geita kupitia Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na GGML umehitimisha program iliyokuwa na lengo la kutoa elimu kwa Jamii juu ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu.
Na: Ester Mabula:
Programu ya kutoa elimu kwa jamii juu ya kukabiliana na uhalifu, iliyokuwa ikiendeshwa na Jeshi la Polisi kupitia Kamisheni ya Polisi Jamii kwa ufadhili wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), imehitimishwa rasmi kwa mafanikio makubwa.

Mpango huu ambao ulikuwa na lengo la kuongeza uelewa wa wananchi juu ya mbinu bora za kujilinda na kushirikiana na vyombo vya dola katika kupambana na uhalifu, umefikia tamati baada ya kufanyika kwa mfululizo wa warsha, mikutano ya hadhara na vipindi vya uelimishaji katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Geita.
Akizungumza katika hafla ya kufunga programu hiyo, Kamishna wa Polisi Jamii nchini Faustine Shilogile ameeleza mafanikio yaliyopatikana ni ushahidi wa nguvu ya ushirikiano kati ya vyombo vya dola na wadau wa maendeleo pamoja na wananchi katika kuimarisha usalama wa wananchi.
Katika hatua nyingine ametoa wito kwa baadhi ya watu hususani viongozi wa dini wanaojihusisha na vitendo vya ukatili.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita SACP Safia Jongo ametoa shukrani kwa GGML kuweza kufanikisha program hiyo na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Polisi Jamii ili kufichua vitendo vya uhalifu
Programu hii imekuwa mfano bora wa jinsi ushirikiano kati ya sekta binafsi na vyombo vya usalama unavyoweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii, hasa katika maeneo yenye changamoto ya kiusalama.
