Storm FM

Mgodi wa Buckreef kutekeleza miradi ya CSR ya 420m

10 April 2025, 7:35 pm

Zoezi la utiaji saini katika hafla iliyofanyika katika ofisi za mkuu wa mkoa wa Geita. Picha na Ester Mabula

Miradi ya CSR (Corporate Social Responsibility) hufanywa na kampuni kama sehemu ya kuwajibika kijamii, kwaajili ya kusaidia jamii inayowazunguka au kulinda mazingira. Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa kampuni haifanyi tu biashara kwa faida, bali pia inatoa mchango chanya kwa jamii.

Na: Ester Mabula:

Halmashauri ya wilaya ya Geita na Mgodi wa Buckreef (BMC) wamesaini mkataba wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) kwa mwaka wa fedha 2024/2025 wenye thamani ya shilingi milioni 420.

Hafla hiyo ya utiaji saini imefanyika leo  Aprili 10, 2025 katika Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Geita na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa, halmashauri na wawakilishi kutoka Mgodi wa Buckreef.

Akizungumza katika hafla hiyo, Ndg. Charles Kazungu ambaye ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Geita ameeleza kuwa fedha hizo zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya kipaumbele katika kata tano za Rwamgasa, Kaseme, Butundwe, Butobela na Busanda ambapo asilimia 60 ya fedha hizo zitatumika katika ngazi ya halmashauri.

Sauti ya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Geita
Mwakilishi Mgodi wa Buckreef, Isaka Bisansaba ambaye ni Kaimu meneja mkuu . Picha na Ester Mabula

Mwakilishi wa Mgodi wa Buckreef, Bw. Isaka Bisansaba ambaye ni Kaimu meneja mkuu wa Mgodi ameipongeza serikali ya mkoa wa Geita kwa kusimamia vyema utekelezaji na maendeleo ya miradi ya CSR.

Sauti Kaimu meneja mkuu wa Buckreef

Diwani wa Kata ya Rwamgasa Joseph Samembe Kaparatus amesema uwepo wa mgodi huo katika kata yake umeendelea kuneemesha wananchi kutokana na utatuzi wa changamoto mbalimbali.

Sauti ya Diwani wa kata ya Rwamgasa
Mkuu wa wilaya ya Geita Hashim Komba akizungumza katika hafla hiyo. Picha na Ester Mabula

Mkuu wa wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba ameupongeza Mgodi wa Buckreef kwa kuendelea kukamilisha miradi ya uwajibikaji kwa Jamii kwa wakati na kueleza kuwabimekuwa muhimu katika kuleta chachu ya maendeleo katika wilaya na mkoa wa Geita.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Geita

Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela amesema kuwa utekelezaji wa CSR ni takwa la kisheria la kampuni kurejesha kwa Jamii na kutoa pongezi kwa Buckreef kwa kitijhada za ukamilishaji wa miradi hiyo kwa wakati.

Sauti ya mkuu wa mkoa wa Geita
Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela akizungumza katika hafla. Picha na Ester Mabula

Miradi itakayotekelezwa kwa fedha hizo ni pamoja na ukamilishaji wa Kituo cha Afya Rwamgasa wenye tthamani ya shilingi 100,000,000,  ujenzi wa barabara kutoka Kasesa – Idoselo na Mnekezi – Kampala  katika kata ya Kaseme  wenye thamani ya shilingi 100,000,000 pamoja na  ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa katika shule ya msingi Lubanda katika kata ya Kaseme wenye thamani ya shilingi 60,000,000.