Storm FM
Storm FM
7 April 2025, 11:49 am

“Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha huduma za Afya zinakuwa bora kwa kila mwananchi” – Barnabas Mapande
Na: Kale Chongela:
Serikali imenunua vifaa tiba vya kisasa na kuongeza madaktari kwenye Kituo cha Afya Nyarugusu wilayani Geita kinachohudumia zaidi ya kata tatu ili kuwaondolea changamoto wananchi ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 38 kufuata huduma hizo hospitali ya wilaya.
Akitoa taarifa ya Kituo hicho mbele ya Jumuiya ya wazazi ya CCM wilaya ya Geita iliyotembelea katika kituo hicho ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya wazazi, Kaimu mganga mfawidhi wa kituo hicho Dkt Fedrick Felician amesema serikali imewapatia vifaa vya kisasa ikiwemo mashine ya Utra sound, mashine ya kinywa na meno ambazo zimekuwa msaada kwa wananchi wa eneo hilo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi wilaya ya Geita Robert Nyamaigolo na Katibu wa malezi na mazingira wa Jumuiya hiyo Paschal Mapung’o wameipongeza serikali kwa hatua hiyo kwakuwa Kituo hicho kinahudumia watu zaidi ya Elfu 70.
Baadhi ya wanawake ambao tayari wamepata huduma katika kituo hicho wametumia fursa hiyo kuipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuwajali wananchi sambamba na kupongeza utoaji wa huduma katika kituo hicho.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Geita Barnabas Mapande amewataka watumishi wa kituo hicho kutumia vifaa hivyo kuwasaidia wananchi kwa kuwa ndiyo dhamira ya serikali.
