

24 March 2025, 3:11 pm
Wajasiriamali waliopo katika soko la asubuhi Nyankumbu kata ya Nyankumbu, katika halmashauri ya manispaa ya Geita wamedai kutoridhishwa na utaratibu unaofanyika wa ugawaji wa maeneo ya kuuzia bidhaa.
Na: Kale Chongela – Geita
Wakizungumza na Storm FM leo Machi 24, 2025 wamesema kuwa jambo hilo limeibuka mara baada ya baadhi ya wajasiriamali kukosa maeneo licha ya kufuata utaratibu uliowekwa ikiwemo kulipia eneo ambalo wanatakiwa kufanyia biashara.
Mmoja wa wajasiriamali aliyepata kibanda katika eneo amesema waliopata ni wale ambao tayari wamefanya malipo kiasi cha shilingi elfu 45 kwa miezi mitatu.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo wilaya ya Geita amepongeza uwepo wa vibanda hivyo na kueleza kuwa changamoto mbalimbali zilizobainika katika ugawaji vibanda zinaendelea kutatuliwa.
Mkurugenzi mtendaji wa manispaa ya Geita Yefred Myenzi akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wetu amesema kuwa taarifa alizonazo ni kwamba zoezi linaendelea vizuri na kwamba hajapokea malalamiko juu ya suala hilo.