

20 March 2025, 12:13 pm
Katika hali ya kushangaza mwanafunzi wa shule ya msingi mwenye umri wa miaka 10 amekuwa akifanyiwa vitendo vya ubakaji kwa zaidi ya mwezi mmoja na watu wawili akiwemo mwalimu wake.
Na: Emmanuel Twimanye – Sengerema
Jeshi la Polisi wilayani Sengerema mkoani Mwanza linawashikilia watu wawili akiwemo mwalimu wa shule ya msingi Daud Ochieng (37) na Adon Sospeter (53) wakazi wa kata ya Ibisabageni kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi (10) wa shule ya msingi Bukala Wilayani Sengerema kwa nyakati tofauti.
Akizungumzia tukio hilo mtoto aliyedaiwa kubakwa akiwa amelazwa katika hospitali teule ya wilaya ya Sengerema amekiri kubakwa na watu hao kwa nyakati tofauti .
Mama mzazi wa mtoto huyo amesikitishwa na tukio hilo na kueleza kuwa baada ya kugundua afya ya mtoto wake imedhoofika ndipo aliamua kumpeleka hospitalini kwa ajili ya uchunguzi huku akitupa lawama kwa watuhumiwa hao.
Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Mwanza Wibroad Mutafungwa amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa wote wawili na wapo mahabusu katika kituo cha Polisi wilayani Sengerema na kwamba watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria mara baada ya uchunguzi wa tukio hilo kukamilika.