

19 March 2025, 4:42 pm
Ikiwa leo imetimia miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, wakazi wa mtaa wa Mbabani kata ya Mtakuja, halmashauri ya manispaa ya Geita wamshukuru kwa kuwajengea shule ya sekondari.
Na: Ester Mabula – Geita
Viongozi na wananchi wa mtaa wa Mbabani kata ya Mtakuja, halamshauri ya manispaa ya Geita wamepongeza na kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuwajengea shule ya sekondari katika mtaa huo.
Hayo yameelezwa leo Marchi 19, 2025 katika ziara ya mkuu wa wilaya ya Geita ya kutembelea miradi ambayo imetekelezwa na Rais Samia Suluhu katika kipindi cha miaka minne madarakani.
Akitoa taarifa ya shule hiyo, mkuu wa shule Jackson Omolo amesema wanashukuru uwepo wa shule hiyo kwani pia wameendelea kupata neema kwa kupatiwa walimu wa masomo ya sayansi sambamba na uboreshewaji wa miundombinu ya shule.
Mmoja wa wanafunzi akizungumza kwa niaba ya wengine ameeleza kuwa, awali walikuwa wakipata shida na wanafunzi wengine kutoendelea na masomo kutokana na umbali wa kwenda shule jirani.
Diwani wa kata ya Mtakuja Mhe. Costantine Morandi amesema shule hiyo imekuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa mtaa wa Mbabani na kwamba imepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya utoro kwa wanafunzi.
Mkuu wa wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba ameeleza kuwa, serikali inaendelea kuikumbuka sekta ya elimu kwa kuhakikisha inajenga shule katika kila eneo na kuwaomba wananchi kuendelea kumuombea Rais afya njema ili aendelee kuleta maendeleo.