

19 March 2025, 4:00 pm
Leo Marchi 19, 2025 imetimia miaka minne ya uongozi wa Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo katika kipindi hicho miradi mbalimbali ya kimkakati imeanzishwa wilayani Geita.
Na: Ester Mabula – Geita
Wananchi wilayani na mkoani Geita wanatarajia kunufaika na mradi mkubwa wa maji ambao unasimamiwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Geita (GEUWASA) ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka huu 2025.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Geita GEUWASA Mhandisi Frank Chanagawa leo Marchi 19, 2025 akizungumza katika ziara ya mkuu wa wilaya ya Geita Mhe. Hashim Abdallah Komba ambayo imetembelea miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya sita.
Mkurugenzi Changawa amesema mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 120 ulianza kutekelezwa April 11, 2023 chini ya mkandarasi na kampuni ya Afcons unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka huu na ambapo utaondoa changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Geita kwa asilimia 100.
Mkuu wa wilaya ya Geita Mhe. Hashim Abdallah Komba amesema dhamira ya serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwani serikali imeendelea kupeleka fedha katika maeneo mbalimbali ndani ya wilaya na mkoa wa Geita ili kukamilisha miradi inayotekelezwa na RUWASA pamoja na GEUWASA.
Ikumbukwe March 17, 2021 Taifa la Tanzania lilipata pigo la kumpoteza Rais Dkt. John Magufuli na March 19 mwaka huo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akaapishwa kuwa Rais wa awamu ya sita wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania na leo March 19, 2025 imetimia miaka minne ya uongozi wake.