Storm FM

Wananchi walalamika kichaka kugeuzwa dampo Geita

8 March 2025, 11:49 am

Muonekano wa eneo ambalo taka zinatupwa. Picha na Kale Chongela

Licha ya jitihada zinazofanywa na uongozi wa manispaa ya Geita wa kuweka mazingira safi na salama, bado baadhi ya wananchi wameendeleza tabia ya utupaji taka kiholela katika mazingira yasio rasmi.

Na: Kale Chongela – Geita

Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Elimu kata ya Nyankumbu Manispaa ya Geita wamelalamikia changamoto ya baadhi ya wananchi kutupa taka ngumu katika eneo ambalo lipo wazi hali inayopelekea uchafuzi wa mazingira

Hayo yameelezwa Marchi 07, 2025 na baadhi ya wananchi wa eneo hilo  ambapo wamebainisha kuwa licha ya eneo hilo kuwa katikati ya makazi ya watu wamekuwa wakikuta taka hizo zimetupwa na kueleza kuwa watu hao wamekuwa wakitupa nyakati za usiku.

Sauti ya wananchi

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo Bw. Hassan Mshora amekiri kuwepo kwa hali hiyo na kueleza kuwa wanatarajia kuanza kufanya ulinzi katika eneo hilo ili kubaini wanaotupa taka ngumu katika eneo hilo.

Sauti ya mwenyekiti Bw. Hassan Mshora

Hata hivyo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya manispaa ya Geita Yefred  Myenzi amesema wana mpango wa kuwanyang’anya maeneo watu wambao wametelekeza maeneo yao na kutoyaendeleza jambo ambalo linapelekea baadhi ya watu kuyatumia kwa kutupa taka.