

4 February 2025, 12:42 pm
Wazazi waambulia patupu baada ya kufanya maandalizi ya shule kwa watoto wao ili hali hawajachaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.
Na Mrisho Sadick:
Serikali ya mtaa wa Nyamakale Kata ya Nyankumbu Manispaa ya Geita Mkoani Geita imeahidi kushirikiana na wazazi wa watoto ambao hawakuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu kutokana na alama zao kuwa chini ya wastani kuhakikisha wanarudia shule ili kutimiza ndoto zao.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo Henry Peter amesema hayo kufuatia changamoto ya baadhi ya wazazi katika mtaa huo kufanya maandalizi ikiwemo kuwashonea sare za shule ya sekondari mkolani iliyopo katika mtaa huo nakuwanunulia vifaa watoto wao ili hali hawajachaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule hiyo kutokana na ufaulu wao kuwa chini ya wastani ambapo ameahidi kuwasaidia ili watoto hao waweze kurudia shule.
Storm FM imefika katika familia mbili zilizopo mtaa wa Nyamakale na Buchundwankende mjini Geita ambazo zilifanya maandalizi ya shule kwa watoto wao ambapo wazazi hao wamesema walipata taarifa kutoka kwa watoto wao kuwa wamefaulu ndio wakaanza kufanya maandalizi hayo wakati huku wazazi wengine wakisema matokeo ya kwanza yaliyotolewa kwa pamoja waliofaulu na kufeli yaliwachanganya wakadhani wamefaulu.
Mkuu wa shule ya sekondari Mkolani bila kurekodiwa amekiri kuwepo kwa wazazi waliyokuwa wakipeleka watoto wao ambao wahawajachaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza licha ya shule hiyo kuwapatia fomu za kujiunga na shule hiyo ambazo zilitolewa kimakosa huku afisa elimu taaluma Mkoa wa Geita Kasian Luoga akizungumza kwa njia ya simu amesema watoto ambao hawajafaulu wamepata chini ya alama 120 huku akiwataka wazazi wa watoto hao kutokata tamaa kwakuwa wananafasi ya watoto wao kurudia shule huku akifafanua madaraja ya ufaulu.