

31 January 2025, 11:56 am
Madiwani waishauri halmashauri ya Nyangh’wale kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato kwa kubuni vyanzo vipya ambavyo haviwaumizi wananchi.
Na Mrisho Sadick:
Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale Mkoani Geita imeendelea kufanya vizuri kwenye ukusanyaji wa mapato kwa miaka mitano mfululizo hali ambayo inaifanya wilaya hiyo kuimarisha huduma za jamii ikiwemo kutekelezaji miradi ya kimkakati kwa ajili ya wananchi.
Hayo yamebainishwa katika kikao maalumu cha Baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo cha mapitio ya bajeti ya mwaka 2023/2024, 2024/2025 na mapendekezo ya bajeti ya Bilioni 4.3 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo kwa kauli moja baraza hilo limepitisha bajeti hiyo.
Akiwasilisha mapendekezo ya bajeti hiyo afisa mipango wa halmashauri hiyo Utali Makwea amesema halmashauri imefanya vizuri kwenye ukusanyaji wa mapato kwa miaka mitano mfululizo huku diwani wa kata ya kharumwa Leonard Mugema akishauri kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato kwenye vyanzo ambavyo vimesahaulika kama mikokoteni ya punda na ng’ombe inayobeba mazao ya biashara na madini ujenzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Husna Tony ameliahidi Baraza hilo kuendelea kufanya kazi kwa nguvu zote huku Mkuu wa wilaya hiyo Grace Kingalame akilitaka baraza hilo kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutangaza mazuri yote anayoyafanya huku mbunge wa jimbo hilo Nossoro Kasu akiahidi kuipigania bajeti hiyo bungeni ili iweze kukubaliwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Isack John ameagiza kufanyiwa kazi mapendekezo yote yaliyowasilishwa katika bajeti hiyo huku akisisitiza suala la ukusanyaji wa mapato.