

31 January 2025, 11:23 am
Shule hiyo ya Bukwimba imeweka rekodi ya kuwa shule ya kwanza katika wilaya hiyo kufaulisha zaidi nakundoa sifuri.
Na Mrisho Sadick:
Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale Mkoani Geita Grace Kingalame ameahidi kutoa zawadi ya Ng’ombe katika shule ya sekondari Bukwimba wilayani humo baada ya shule hiyo kufanya vizuri kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ikiwemo kutokomeza zero.
Kingalame akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo amefika katika shule ya sekondari ya Bukwimba ambayo imeweka rekodi ya kuwa shule ya kwanza tangu kuanzishwa kwa wilaya hiyo kufaulisha wanafunzi 48 kwa daraja la kwanza , daraja la pili 32 , daraja la tatu 35 na daraja la nne wa 3 na hakuna waliopata sifuri.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Nyagh’wale John Isack amesema shule hiyo hapo awali ilikuwa ikikabiliwa na changamoto rukuki baada ya serikali kuzifanyia kazi ndio sababu ya ufaulu mzuri huku akiahidi kutoa gunia moja la mpunga kwa wanafunzi hao.
Mkuu wa shule hiyo Richard Mgole amesema kilichosababisha ufaulu huo mzuri ni pamoja na kila mwalimu kutambua wajibu wake pamoja na mikakati ambayo walijiwekea kuhakikisha wanatokomeza sifuri na imewezekana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Husna Tony amesema Ufaulu umepanda kwa asilimia 6.42 nakwamba Wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato Cha nne mwaka 2024 walikuwa 1,294 Kutoka kwenye shule 12 za sekondari, wanafunzi waliofaulu kuanzia daraja la kwanza hadi la nne ni 1,201 sawa na asilimia 92.8 ukilinganisha na Ufaulu wa mwaka 2023 ambao ulikuwa ni asilimia 86.2.