Sekondari ya Lutozo kuondokana na changamoto ya maji
15 October 2024, 2:56 pm
Shule ya sekondari Lutozo iliyopo kata ya Katoro halmashauri ya wilaya ya Geita imeondokana na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama baada ya wadau wa maendeleo kushirikiana na serikali kuchimba kisima.
Na: Edga Rwenduru – Geita
Wanafunzi wa shule ya sekondari Lutozo iliyopo halamsahauri ya wilaya ya Geita kuondokana na adha ya ukosefu wa maji katika shule hiyo baada ya ujenzi wa kisima chenye thamani ya shilingi milioni 16.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi wakati wa mahafari ya kidato cha nne iliyofanyika Oktoba 11, 2024, mkuu wa shule hiyo Revocatus Maraha amesema changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama ni ya muda mrefu na walimu walikuwa wanalazimika kuwaagiza wanafunzi kwenda na maji kutoka nyumbani kwao.
Wanafunzi wa kike katika shule hiyo ndio waliokuwa wakiathirika zaidi na ukosefu wa maji kama ambavyo baadhi ya walimu wa shule hiyo wanavyobainisha zaidi.
Katibu mkuu wa chama cha walimu Tanzania CWT Joseph Misalaba ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya mdau wa maendeleo katika mkoa wa Geita Kulwa Biteko amesema ukosefu wa maji safi na salama kwa wanafunzi unaweza kuwa chanzo cha kushusha taaluma kwa wanafunzi.
Naye diwani wa kata ya Katoro Kigogo Sweya ametumia frusa hiyo kuwaomba wadau wa elimu pamoja na wafanyabiashara kushirikiana na serikali kuboresha miundombinu ya shule zinazopatikana katika kata hiyo.