Rafiki Trustee Team yatoa msaada wa vifaa vya shule kwa wanafunzi
8 October 2024, 2:55 pm
Baadhi ya watoto waishio katika mazingira magumu na kaya duni wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mahitaji ya shule.
Na: Evance Mlyakado – Geita
Wanafunzi 46 kutoka shule za msingi na sekondari tano ndani ya wilaya ya Geita wamepokea msaada wa mahitaji ya shule kutoka kwa mwalimu wa taaluma mwandamizi katika shule ya sekondari Ludete akishirikiana Rafiki Trustee Team kutokana na baadhi yao kushindwa kuhudhuria masomo.
Akizungumza na Storm FM Oktoba 7, 2024 wakati wa hafla ya kuwapatia msaada wa mahitaji hayo ya shule mwalimu Juma Lukanula amesema msukumo wa kuwasaidia wanafunzi hao mahitaji ya shule umetokana na ukweli kwamba baadhi yao wanaishi katika mazingira magumu.
Aidha katika hatua nyingine Lukanula amewataka watanzania kuwa na moyo wa kuwasaidia wenye uhitaji kutokana na uwepo wa kundi kubwa la wanafunzi wanaoshindwa kutimiza ndoto zao.
Baadhi ya wanafunzi waliopatiwa mahitaji hayo ya shule wamemshukuru mwalimu huyo pamoja na Rafiki Trustee Team kwa kuwawezesha mahitaji hayo huku wakiahidi kujituma katika masomo yao.
Kwa upande wake mmoja wa wazazi waliohudhuria katika hafla hiyo amewashukuru na kuipongeza Rafiki Trustee Team chini ya mwalimu Lukanula huku akiwataka kuendeleza kile walichokianzisha kwa jamii yote. bila ubaguzi.
Wanafunzi hao kutoka shule za sekondari Ludete, Bugayambelele, Katome na shule za msingi Mji mwema na Ludete wamepatiwa sare za shule, madaftari, mabegi ya shule, viatu na sukari kilo mbili kwa kila mmoja.