Wachimbaji waomba mgodi uliofungwa ufunguliwe Mbogwe
26 September 2024, 4:14 am
Baadhi ya wananchi mkoani Geita wamekuwa wakijihusisha na shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu ili kuendesha maisha yao pamoja na kupata kipato cha kumudu gharama za maisha.
Na: Edga Rwenduru -Geita
Wachimbaji wadogo katika mgodi wa Isanjabhadugu (maarufu Area B) uliopo kata ya Nyakafuru wilayani Mbogwe mkoani Geita wameiomba serikali kupitia ofisi ya mkoa wa Geita kuufungua mgodi huo ambao ulifungwa baada ya mpasuko uliotokea katika eneo hilo ambao ulikuwa unahatarisha maisha ya wachimbaji hao.
Wametoa maombi hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela Septemba 23, 2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.
Baadhi ya viongozi akiwemo makamu mwenyekiti wa wachimbaji wa Isanjabhadugu, Sangundi Mpigahodi amesema eneo hilo halifai kwa uchimbaji na sio salama kwa maisha ya binadamu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amemwagiza afisa madini wa mkoa wa kimadini Mbogwe, wamiliki wa leseni pamoja na wachimbaji kufanya kikao cha mapendekezo ili kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.