Wanaoeneza uvumi watoto kutolewa figo waonywa Geita
19 September 2024, 10:14 am
Inadaiwa uwepo wa taarifa za uongo juu ya matukio ya watoto kutekwa nakutolewa figo imeendelea kuleta taharuki katika jamii huku vyombo vya dola vikitakiwa kusimama kidete.
Na Mrisho Sadick:
Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Geita imewaonya baadhi ya watu wanaoendelea kueneza uvumi juu ya uwepo wa vitendo vya wizi wa watoto kwa ajili ya kwenda kuuzwa nakutolewa figo hali ambayo inaleta taharuki katika jamii wakati siyo kweli.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Jumuiya hiyo wilaya ya Geita Ramadhani Abdalah baada ya kumalizika kwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanachama wake wa Kata ya Kalangalala halmashauri ya mji wa Geita ambapo amesema taarifa hizo za uongo zinaleta hofu hali ambayo inawafanya baadhi ya wananchi kujichukulia Sheria mkononi nakuleta athari kwa watu wasiyo husika.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kalangalala Fortunatus Emmanuel watu wanaoeneza taarifa hizo wana ajenda zao za kuichafua serikali nakwamba hana taarifa ya matukio ya watoto kutekwa nakutolewa figo huku akiwataka wananchi wasiwe na hofu.
Baadhi ya Wazazi katika Halmashauri ya mji wa Geita Jumanne Bansabe na Merry Mpangalala wameiomba serikali kuendelea kuwatafuta nakuwachukulia hatua kali baadhi ya watu wanaosambaza taarifa za uongo ikiwemo kupitia Mitandao ya kijamii.
Matokeo ya athari ya taarifa hizo za uongo iligharimu maisha ya watu wawili wilayani Mbogwe Mkoani Geita hivi karibuni baada ya wananchi kuandamana kwenda kituo cha polisi Lulembela kutaka kuwachukua kwa nguvu watuhumiwa wa wizi wa watoto ili hali walikuwa siyo wezi nakusababisha vurugu kubwa na watu wawili wasiyo kuwa na hatia kufariki.