Storm FM

Watatu wahukumiwa kifo mauaji ya Milembe Geita

28 August 2024, 1:50 am

Watuhumiwa wanne wa kesi ya mauaji ya Milembe Suleiman wakisikiliza hukumu ya kesi hiyo. Picha na Daniel Magwina

Washtakiwa watatu kati ya wanne (wa kwanza kulia, wa kati na dada wa nyuma) waliokuwa wakishtakiwa kwa kosa la mauaji ya Milembe Suleiman (43) wametiwa hatiani kwa kutenda kosa hilo na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Na: Daniel Magwina – Geita

Hukumu hiyo iliyoanza kusomwa saa 3:02 hadi saa 5:12 asubuhi a Agosti 27, 2024 na Jaji mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Geita Kelvin Mhina ameeleza kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka Mahakama imewatia hatiani washtakiwa wakwanza hadi wa tatu na kumuachia huru mshtakiwa wa nne Musa Lubingo.

Waliotiwa hatiani katika kesi hiyo namba 39 ya mwaka 2023 ni Dayfath Maunga (30), Safari Lubingo (54), na  Genja Deus Pastory.

Akitoa hukumu hiyo Jaji Mhina ameeleza mambo muhimu ya kuzingatia ni kama kweli Milembe alifariki, kifo kilikuwa cha kawaida au la,walioshtakiwa kama ndio waliohusika  na kama mauji hayo yalikuwa yakukusudia.

Ameeleza kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo hakuna ubishani kuwa Milembe alifariki na mwili wake kukutwa na majeraha kama ulivyothibitishw ana shahidi wa sita aliyekua daktari aliyeufanyia mwili uchunguzi.

Mbali na daktari aliyethibitisha kwa kutoa hati ya uchunguzi wa mwili pia shahidi wa nne aliyekuwa mwenyekiti wa mtaa wa Mwatulole alithibitisha kuukuta mwili kwenye nyumba zilizokuwa zinajengwa hivyo hakuna shaka kuwa Milembe alifariki.

Kuhusu kifo kisicho cha kawaida Jaji ameeleza kwa taarifa ya daktari inayoeleza majeraha yenye sentimita 14, 8 na 6 aliyoyapata katika maeneo ya kichwani, shingoni na mkononi inaonyesha marehemu alifikwa na umauti kwa njia ya kikatili sana.

Amedai kwa mujibu wa ushahidi kifo cha marehemu hakikuwa cha kawaida  na kuhusu nani alimuua ushahidi upo kwenye vina saba ,ripoti ya uchunguzi , CCTV, pamoja na maelezo ya washtakiwa.

Jaji Mhina ameeleza ushahidi wa DNA wa damu uliochukuliwa kwenye jambia lililotumika kumuua Milembe, matokeo yanaonyesha damu iliyokutwa kwenye jambia ni ya mwanamke huku mate na damu iliyochukuliwa kwenye mpini  wa Jambia ilikuwa ya mtu mmoja mwanaume ambae ni mshtakiwa wa tatu.

Jaji Mhina ameeleza ushahidi wa shahidi wa 22 na 28 unaongeza uzito wa ushahidi wa DNA na pale mshtakiwa wa tatu alivyoletwa Geita na  kuonyesha jambia lililotumika kumuua pamoja na simu za marehemu.

Ameeleza ushahidi uliotolewa na shahidi wa tano juu ya alama za vidole zilizokutwa kwenye chupa zilibainika kuwa  za mshtakiwa wa tatu  na kwa mujibu wa wataalamu hakuna alama za vidole zinazofanana na za mwingine.

Amedai pia katika maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu Genja Deus Pastory  alikiri na kueleza namna alivyotupa silaha na simu za marehemu na Mei 6, 2023 aliwaongoza askari na kwenda kuwaonyesha maeneo alikotupa Jambia na simu.

Ameeleza kwa mujibu wa DNA ya alama za vidole na kitendo cha yeye kuwapeleka askari eneo alikotupa  simu na Jambia vinaunga mkono maelezo ya onyo aliyoyatoa licha ya kuwa maelezo hayo aliyakataa.

Jaji Mhina ameeleza katika ushahidi uliotolewa kwenye maelezo ya onyo mshtakiwa namba 3 amekiri kuwa yeye ndiye alimkata marehemu kichwani.

Kuhusu mshtakiwa wa kwanza shahidi wa 11 ambaye aliandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo alikiri kupanga kutafuta wauaji na alikiri kuishi na marehemu kama mume na mke na kuwa alikuwa akinyanyaswa na alitaka kuondoka lakini ilishindikana.

Katika ushahidi huo unaeleza namna alimtafuta mshtakiwa wa pili Safari Lubingo aliyewatafuta washtakiwa wengine  akiwemo Genja Deus Patory na kuwalipa kiasi cha Tsh milioni 2.6.

Amedai pamoja na mshtakiwa kudai hakuandika maelezo ushahidi huo unaangalia kama kuna ushahidi mwingine wa kuunga mkono maelezo yaliyokataliwa na kuwa ushahidi wa mazingira unaongeza nguvu kwenye ushahidi wa maelezo ya onyo.

“Mshtakiwa alikamatwa Mei mosi na yeye ndiye aliyemtaja mshtakiwa wa pili na kueleza anakoishi na shahidi wa 24 ameeleza alivyomkamata shahidi wa pili na bila mshtakiwa wa kwanza kutoa taarifa mshtakiwa wa 2, 3 na wa nne wasingekamatwa kwa mazingira hayo ushahidi unaunga ushahidi wa mshtakiwa wa 1&2” amesema.

Ameeleza licha ya kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha washtakiwa kutenda kosa hilo au kuwa eneo la tukio lakini mshtakiwa wa 1 & 2 wao ndio walipanga mauaji na mshtakiwa wa kwanza ndiye aliyelipa wauaji.

Jaji Mhina amedai kwa mujibu wa sheria anaesaidia au kutafuta muuaji anakuwa na hatia ya kusababisha kifo.

Kuhusu mshtakiwa wanne Jaji ameeleza kuwa mshtakiwa huyo kwa mujibu wa shahidi wa nane wa upande wa mashtaka mshtakiwa huyo alijitoa kwenye hatua za awali  na hakuhusika tena na mauji hayo.

Kufuatia ushahidi huo Jaji Mhina ameeleza upande wa mashtaka umethibitisha kosa kwa mshtakiwa wa 1,2 na wa tatu kuwa walitenda kosa kinyume na kifungu cha 196 &197 sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Mwendesha mashtaka wa serikali Scolastica Teffe amedai hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya washtakiwa hao huku wakili wa upande wa utetezi Laurent Bugoti ameiomba Mahakama kutoa hukumu kwa mujibu wa sheria kwa kuwa hakuna mbadala wa adhabu ya kesi ya mauaji.

Akitoa hukumu hiyo Jaji Mhina ameeleza kwa mujibu wa sheria washtakiwa hao wanahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa mshtakiwa wa 1,2 na wa tatu na kuwaeleza wana haki ya kukata rufaa endapo hawajaridhika na hukumu hiyo.