Storm FM

Wakazi Narusunguti wilayani Bukombe wajengewa zahanati

19 July 2024, 5:05 pm

Jengo la zahanati ya Narusunguti wilayani Bukombe ambalo limejengwa. Picha na Evance Mlyakado

Zaidi ya milioni 100 kutoka mfuko wa TASAF wilaya ya Bukombe zimesaidia ujenzi wa jengo la Zahanati ya kijiji cha Narusunguti kilichopo kata ya Busonzo hapa mkoani Geita.

Na: Evance Mlyakado – Geita

Ujenzi wa zahanati hiyo ni kufuatia adha ya muda mrefu ya wakazi wa Narusunguti kata ya Busonzo wilayani Bukombe mkoani Geita kutembelea umbali mrefu kufata huduma za afya katika vijiji jirani.

Akizungumza na Storm fm mara baada ya kufanya ukaguzi wa jengo la zahanati hiyo, Afisa Afya kutoka ofisi ya Mganga mkuu wa wilaya ya Bukombe, William Mayila Sango ameupongeza uongozi wa kijiji hicho kutokana na usimamizi mzuri wa fedha hizo na kueleza wanatarajia huduma zitaanza kutolewa Julai 30, mwaka huu.

Sauti ya afisa afya

Afisa mtendaji wa kijiji hicho Herman Martine Misinzo na mwenyekiti wa kijiji Kasema Mashauri Lukaga wameahidi kufanyia kazi maelekezo yaliyotolewa kabla ya muda uliopangwa ili zahanati hiyo izinduliwe na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Sauti ya mtendaji na mwenyekiti

Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamesema wanatembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika kituo cha afya Uyovu na zahanati binafsi zilizopo vijiji jirani na kwamba kufunguliwa kwa zahanati hiyo kutawaondelea changamoto hiyo.