Mwanafunzi ajeruhiwa kwa viboko kutokana na utoro Geita
17 July 2024, 10:41 am
Licha ya waraka wa elimu Na. 24 wa mwaka 2002 kuelekeza utolewaji wa adhabu ya viboko kwa wanafunzi, utolewaji wa adhabu hiyo umekuwa ukikiukwa.
Na: Nicolaus Lyankando -Geita
Mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Kisesa halmashauri ya mji wa Geita mkoani Geita anadaiwa kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa viboko na walimu kwa kushirikiana na mzazi wake.
Akizungumzia tukio hilo mtoto huyo (15) mkazi wa Nguzo Mbili katika kata ya Mwatulole mjini Geita amesema kitendo hicho amefanyiwa asubuhi ya Julai 15, 2024 baada ya kufika shuleni na kuanza kuchapwa viboko na walimu wake wakishirikiana na baba yake mzazi na kubainisha amechapwa viboko zaidi ya 20.
Kwa upande wake mzazi wa mtoto huyo amekiri kumwadhibu mtoto wake akiwa shuleni huku mmoja ya walimu waliomwadhibu akidai walimwadhibu baada ya mtoto huyo kuwa na tabia ya kutoroka shuleni na kutoingia darasani.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Shilabela Bw. Fredrick Masalu ambapo ndipo eneo ambalo mtoto huyo aliokotwa akiwa katika hali hiyo ya majeraha ya viboko ameeleza juu ya namna alivomuona mwanafunzi huyo.
Waraka wa Elimu Na. 24 wa mwaka 2002 unaelekeza kuwa adhabu ya viboko kwa mwanafunzi itolewe na mwalimu mkuu au mwalimu mwingine atakayeteuliwa na mwalimu mkuu kwa maandishi kila mara kosa linalostahili adhabu hii litatendeka.