Storm FM

Jodade yawajengea uwezo watoto na vijana Geita

12 June 2024, 11:56 am

Baadhi ya watoto kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini wakiwa kwenye semina ya kuwajengea uwezo mjini Geita. Picha na Mrisho Sadick

Kutokana na kundi la watoto na vijana kuwa katika hatari zaidi ya kuharibikiwa serikali , taasisi za kiraia , wadau na wazazi wameingilia kati kunusuru kundi hilo.

Na Mrisho Sadick:

Jodade Foundation imewakutanisha watoto na vijana kuanzia miaka 12 hadi 35 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za kidunia ikiwemo vitendo vya ukatili na ukuaji wa teknolojia ambao umekuwa ukichangia kuporomoka kwa maadili kutokana na baadhi ya watu kuiga tamaduni za mataifa mengine.

Semina hiyo imefanyika katika Halmshauri ya mji wa Geita mkoani Geita juni 08,2024 huku baadhi ya watoto na vijana walioshiriki katika semina hiyo wamesema licha ya mitandao hiyo kuwa na umuhimu mkubwa lakini matumizi ya simu yanayochangiwa na kukua kwa teknolojia yasipodhibitiwa kwa watoto ni hatari kwao nakwamba elimu waliyoipata kwenye semina hiyo itakwenda kuwasaidia kukabiliana na changamoto hizo kwa wigo mpana.

Sauti ya watoto na vijana
Viongozi wa wilaya na Jeshi la polisi Geita wakiwa katika semina ya watoto na vijana mjini Geita. Picha na Mrisho Sadick

Tafiti zinaonesha kuwa kuna ongezeko la watumiaji wa mitandao na Watoto wakiwa miongoni mwao, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya Watoto duniani wanaweza kutumia mitandao ya simu bila ya idhini au usimamizi wa wazazi jambo ambalo ni hatari kwa watoto na vijana.

Mkurugenzi wa Jodade Foundation Josca Rumanyika akiwa kwenye semina hiyo ameonesha wasiwasi waoke kuhusu ulinzi na usalama wa mtoto kwani wazazi wengi wamekuwa bize hali ambayo imewafanya kusahau kuwekeza kwa watoto huku akiwasisitiza umuhimu wa kuweka mazingira salama ikiwemo ya kuwaruhusu kushiriki katika makongamano na semina ili kuwajengea uwezo.

Sauti ya mkurugenzi wa Jodade Foundation
Jeshi la polisi na viongozi wa wilaya ya Geita wakiwa katika semina ya watoto na vijana mjini Geita. Picha na Mrisho Sadick

Mkaguzi msaidizi wa Jeshi la Polisi wilaya ya Geita  Denis Simba na mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Geita Cosmas Bayaga wameipongeza Jodade Foundation kwa kuendelea kushirikiana na serikali kuwajengea uwezo watoto na vijana nakwamba kuna umuhimu mkubwa wa kuwajengea ufahamu ili kukabiliana na changamoto katika ukuaji wa teknolojia na namna ya kuripoti taarifa za vitendo vya ukatili.

Sauti ya Mkaguzi wa Polisi na Mwakilishi wa DC Geita
Mkurugenzi wa Jodade Foundation Josca Rumanyika akizungumzia semina ya watoto na vijana. Picha na Mrisho Sadick

Jodade Foundation huandaa semina hiyo mara mbili kila mwaka mwezi Juni na Disemba wakati wanafunzi wanapokuwa likizo.