Dkt. Biteko akemea mivutano ya wananchi, TFS
7 June 2024, 11:15 am
Kuchelewa kwa utatuzi wa migogoro ya wananchi na TFS katika maeneo ya hifadhi imeendelea kuleta athari kwa baadhi ya wananchi ikiwemo vifo.
Na Mrisho Sadick – Bukombe
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko amewataka wakazi wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita kuacha kuingia kwenye pori la hifadhi la Kigosimayowosi bila kibali huku akimtaka Kamishna wa TFS kuhakikisha anakomesha vitendo vya askari wake kudaiwa kuwanyanyasa wananchi.
Dkt. Biteko ametoa kauli hiyo Juni 06,2024 kwenye mkutano wa hadhara wa Jimbo lake la Bukombe uliofanyika kwenye Kata ya Igulwa, kutokana na uwepo wa mivutano kati ya askari wa TFS wanaotekeleza sheria ya kulinda eneo hilo na wananchi ambao wanaingia kwenye hifadhi hiyo nakufanya shughuli za kibinadamu bila vibali.
Hifadhi hiyo yenye ukubwa wa kilometa za mraba 13,000, imezungukwa na mikoa minne ya Geita, Tabora, Shinyanga na Kigoma, awali mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Nicholaus Kasendamila ameiomba serikali kuharakisha mchakato wa ugawaji wa eneo la hifadhi hiyo kwa wananchi ambao umeanza muda mrefu kwani kuchelewa huko kunaendelea kuleta migogoro.
Akiwa kwenye mkutano huo Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Dkt Festo Dugange amesema mbali na serikali kutoa milioni 900 kwa ajili ya ukarabati wa Hosptali kongwe ya wilaya pia imetenga milioni 500 kwa ajili ya kujenga Jengo la kisasa la watoto wanaozaliwa kabla ya wakati yaani (Njiti).
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema yeye pamoja na watendaji wa serikali Mkoani humo wataendelea kusimamia fedha zinazotolewa na serikali huku akiwataka watumishi wa umma mkoani humo kuendelea Kusikiliza kero za Wananchi.