Storm FM

Wakazi wa Izunya wadai maji ya sumu yanaua mifugo, kuharibu mazao

27 May 2024, 3:31 pm

Wakazi kijiji cha Mwamakiliga kata ya Izunya wilaya ya Nyang’hwale wakiwa katika mkutano wa mkuu wa mkoa wa Geita. Picha Mrisho Sadick

Licha ya uwepo wa migodi ya uchimbaji wa madini katika maeneo mengi mkoani Geita lakini shughuli hizo zimekuwa mwiba mchungu kwa wakulima na wafugaji katika kata ya Izunya.

Na Mrisho Sadick:

Wakulima na wafugaji wa kijiji cha Mwamakiliga kata ya Izunya wilayani Nyang’hwale mkoani Geita wameiomba serikali kuwachukulia hatua kali baadhi ya wawekezaji wa madini ya dhahabu wanaotiririsha maji yenye sumu kuelekea kwenye mashamba yao na vyanzo vya maji vya asili hali ambayo wanadai imesababisha mifugo yao kufa na mazao kuharibika.

Baadhi ya wakulima na wafugaji hao wametoa kilio chao kwenye Mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Mkoa wa Geita aliyefika kwenye Kata hiyo kukagua miradi ya maendeleo nakusikiliza kero za Wananchi ambapo wamesema maji yaliyochangamana na sumu kutoka katika mialo ya uchenjuaji wa madini ya dhahabu ni hatari kwa usalama wao  mifugo na mazao yao nakuiomba serikali kuingilia kati.

Sauti ya wakulima na wafugaji
Kaimu Afisa Madini wa Mkoa wa kimadini Mbogwe akiwa kwenye mkutano akiwa kwenye mkutano wa mkuu wa mkoa wa Geita. Picha na Mrisho Sadick

Kaimu Afisa Madini wa Mkoa wa kimadini Mbogwe akiwa kwenye mkutano huo amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo bila kueleza ukubwa wa tatizo na athari zilizotokea kwa wananchi amesema walichukua hatua kwa wahusika.

Sauti ya kaimu afisa madini
Mkuu wa mkoa wa Geita akiwa kwenye mkutano na wakazi wa kata ya Izunya Nyang’hwale. Picha na Mrisho Sadick

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela ameiagiza Ofisi ya Madini kuchukua hatua ikiwemo kuwalipa fidia waathirika waliyopoteza mifugo na mazao yao kutokana na sumu hiyo.

Sauti ya mkuu wa mkoa