Waziri Mkuu kutua Geita mwezi Juni
26 May 2024, 4:42 pm
Ili kuongeza ufanisi na wigo katika ukusanyaji wa mapato serikali imeendelea kuanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kutengeneza walipa kodi wapya kupitia vituo hivyo.
Na Mrisho Sadick:
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa anatarajia kuzindua Kituo Cha uwezeshaji Wananchi kiuchumi wilayani Nyang’hwale Mkoani Geita kilichojengwa kwa thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200.
Akitoa taarifa ya Ujenzi wa Kituo hicho mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale Husna Tony amesema mradi huo umefikia asilimia 97 nakwamba kitajumuisha Taasisi zaidi ya 16 ikiwemo TRA , TBS na SIDO.
Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingalame amesema mbali na kituo hicho kuwa maalumu kwa wafanyabiashara lakini wameweka tawi la chuo kikuu huria kwa ajili ya kuwaepusha wakazi wa wilaya hiyo kutoka nje ya wilaya kutafuta elimu ya juu mikoa mingine.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema Kituo hicho kitakuwa na manufaa makubwa kwa wafanyabiashara wa wilaya hiyo nakwamba kitazinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa Juni mosi mwaka huu.