Storm FM

Baada ya kifo cha mjamzito, zahanati yaanza kazi Lubanda

3 May 2024, 11:29 am

Muonekano wa zahanati ya kijiji cha Lubanda. Picha na Edga Rwenduru

Baada ya kupita muda mrefu licha ya zahanati iliyojengwa kwa nguvu za wananchi kushindwa kutoa huduma, hatimaye kilio cha wananchi wa kijiji cha Lubanda kata ya Busanda kimesikika.

Na: Ester Mabula – Geita

Diwani wa kata ya Busanda Selemani Gwamala wakati akifanyiwa mahojiano na kituo cha redio cha Storm Fm katika kipindi cha Storm Asubuhi amesema kuwa kwa sasa kero ya wananchi kutembea umbali mrefu ili kufuata huduma za afya kijiji jirani imekwisha baada ya zahanati hiyo kufunguliwa na kuanza kutoa huduma.

Sauti ya Diwani wa Busanda
Diwani wa kata ya Busanda Selemani Gwamala akizungumza katika studio za Storm FM. Picha na Kale Chongela

Hayo yanajiri kufuatia tukio la mama mjamzito kufariki dunia baada ya kujifungulia njiani wakati anaelekea kituo cha afya Katoro kilicho umbali wa zaidi ya kilometa 10 kutoka kutoka kijiji cha Lubanda kilichopo kata ya Busanda.

Baadhi ya Wakazi wa kijiji cha Lubanda Marietha Thomas , Mayala Magili na Tatu Masele wakielezea tukio hilo waliiomba serikali kuwasaidia zahanati iliyojengwa kwa nguvu za wananchi ianze kufanya kazi.

Sauti ya wananchi wa Lubanda

Katika hatua nyingine diwani Gwamala akizungumzia maendeleo katika kata yake amesema kwa sasa hakuna changamoto ya maji safi na salama kutokana na jitihada zinazochukuliwa za kuhakikisha kila kijiji kina maji safi na salama.

Sauti ya Diwani wa Busanda

Zahanati ya kijjiji cha Lubanda kata ya Busanda imezinduliwa rasmi Mei mosi, 2024 na kwa sasa inaendelea kutoa huduma kwa wananchi wa kijiji hicho.