Ishololo waondokana na adha ya kutembea umbali mrefu
16 September 2023, 1:21 pm
Ubunifu wa ujenzi wa miradi kupitia fedha za TASAF umekuwa na matokeo chanya hususani maeneo ya vijijini ambayo yalikuwa yakikabiliwa na changamoto ya huduma za jamii kama afya, maji na elimu.
Na Mrisho Sadick:
Wakazi wa kijiji cha Ishololo wilayani Bukombe mkoani Geita wameondoka na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya baada ya serikali kupitia fedha za TASAF kutoa Shilingi milioni 102 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika eneo hilo.
Wakizugumzia hatua hiyo baadhi ya wakazi wa kijiji hicho baada ya zahanati hiyo kutembelewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Mhe George Simbachawene wamesema kwa sasa hawatatumia gharama kubwa kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
Baada ya kukagua zahanati hiyo Waziri George Simbachawene ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na kusema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2020 hadi 2023 serikali imepeleka zaidi ya bilioni 7 katika wilaya ya Bukombe kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kujiinua kiuchumi.
Waziri Simbachawene amehitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani Geita katika wilaya Bukombe kwa kutembelea miradi mbalimbali ya TASAF na kuzungumza na wanufaika. Katika ziara hiyo mkoani Geita ametembelea wilaya za Geita , Chato na Bukombe.