Storm FM

Mkoa wa Geita wafikia asilimia 72.1 ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee.

10 August 2021, 3:02 pm

Na Mrisho Sadick:

Mkoa wa Geita umefanikiwa kufikia asilimia 72.1 ya unyonyeshaji maziwa ya mama pekee kwa mwaka wa 2020/21 kwa watoto wa miezi 0 hadi miezi 6 kutokana na jitihada za idara ya Afya kitengo cha Lishe kutoa elimu ya unyonyeshaji kwa jamii kupitia watoa huduma ya Afya.

 Amesema hayo Afisa Lishe mkoa wa Geita Riziki Mbilinyi alipokuwa akizungumza na Geita Press Blog kuhusu hali ya unyonyeshaji katika mkoa wa Geita kwenye wiki ya Unyonyeshaji ambayo hufanyika kila Agosti 1-7 ya kila mwaka.

Aidha alisema hali ya unyonyeshaji mtoto maziwa ya mama kutoka miezi sita mpaka miaka miwili ni asilimia 40.7 ,hii inatokana na baadhi ya akina mama kusongwa na shughuli nyingi za utafutaji pamoja na masuala ya uzazi wa mpango.

Mbilinyi alisema unyonyeshaji imeonekana kuwa afua mojawapo ya kupunguza vifo vya watoto ,kwani mtoto akinyonyeshwa ipasavyo inaongeza kinga ya mwili kwa mtoto.

“Tunashauri watoto kuanzia miezi sita hadi miezi 23 waanzishiwe kunyonya maziwa ya mama mara tu baada ya kuzaliwa katika kisichozidi saa moja ya baada ya mama kujifungua,wapewe mziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwazo baada ya kuzaliwa”alisema Mbilinyi.

Alisema mtoto anaweza kuanzishiwa chakula cha ziada baada ya miezi sita kutokana na kwamba utumbo wake utakuwa umekomaa kwa ajili kupata chakula kingine zaidi ya maziwa.

Mmoja wa wazazi walikutwa kwenye kituo cha Afya Nyankumbu Rebecca James mwenye mtoto wa miezi miwili alisema ,anatambua umuhimu wa elimu wanayopewa na watoa huduma wa Afya  toka mama akiwa mjamzito hadi kujifungua kuhusu suala la unyonyeshaji.

“Kliniki ya kwanza tu nikiwa na mme wangu tuliambia baada ya kujifungua mtoto anatakiwa anyonyeshwe maziwa ya mama pekee hadi atakapofikisha miezi sita..na mimi mwanangu huyu nitafanya hivyo hadi miezi sita ndipo nitaangalia namna kumuzanzia chakula kingine”alisema Rebecca.

Kwa mujibu wa Mwongozo wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii jinsia wazee na watoto kuhusu maadhimisho ya wiki ya unonyeshaji Tanzania imepiga hatua katika unyonyeshaji wa maziwa ya mama ambapo idadi ya wanawake asilimia 98 wamachagua kuwanyonyesha watoto wao.

Pia asilimia 53.5 ya watoto wanaanzishiwa kunyonya maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa.

Aidha,Takwimu pia zinaonyesha kuwa asilimia 58 ya watoto wananyonyeshwa ya mama pekee ndani ya miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa ,Watoto wanaoendelea kunyonyeshwa hadi kufikia umri wa mwaka mmoja ni asilimia 92.2 huku wanaoendelea kunyonyeshwa hadi kufikia miaka miwili ni asilimia 43.