Wananchi walalamikia utupaji wa taka holela Geita
22 January 2025, 2:59 pm
Baadhi ya wananchi wamelalamikia hali ya umwagaji taka holela katika dampo lililopo mkabara na barabara itokayo manispaa ya Geita kuelekea Nzera mkoani Geita.
Na: Kale Chongela – Geita
Wananchi hao wakiwa katika eneo la dampo wamezungumza na Storm FM Januari 21, 2025 na kubainisha kuwa changamoto hiyo inachangia taka kumwagwa kiholela na kupelekea uharibifu wa mazingira karibu na barabara.
Baadhi ya vijana ambao wanajihusisha na uokotaji wa taka ikiwemo chupa na vyuma katika eneo hilo wameeleza changamoto hiyo imekuwa ikijitokeza kutokana na madereva wa gari la taka kutozingatia eneo sahihi la kumwaga taka.
Msimamizi wa uzoaji taka manispaa ya Geita Edigar Onyanga kutoka kampuni ya Gin investment ambayo inasimamia uzoaji taka ngumu manispaa ya Geita, akizungumza kwa njia ya simu amekiri kuwepo kwa hali ya utupaji taka holela katika eneo la dampo na kwamba wapo baadhi ya wafanyabiashara wanaotuma watu binafsi kumwaga taka hizo.
Afisa mazingira manispaa ya Geita Edward Mwita amesema taarifa juu ya changamoto hiyo zipo ofisini kwao na kwamba wameomba fdha kwaajili ya kufanya matengenezo ikiwemo kuweka uzio ili kuzuia utupaji taka holela.