Mashimo ya barabara yawatesa madereva Geita
5 November 2024, 12:16 pm
Miundombinu ya barabara kwa baadhi ya maeneo mkoani Geita imeendelea kuwa na changamoto hali ambayo inapelekea adha kwa watumiaji wa barabara husika.
Na: Kale Chongela – Geita
Madereva wanaotumia barabara ya kutoka mjini Geita hadi Nzera wamedai kukabiliwa na changamoto ya uwepo wa mashimo katikati ya barabara ya kona eneo la Lushanga.
Baadhi ya madereva wa magari wakizungumza na Storm FM Jumatatu Novemba 3, 2024 wamesema kuwa uwepo wa mashimo hayo unawapa wakati mgumu hasa wakati wa kupishana na gari lingine kwani wanalazimika kusimama.
Wakizungumza awtumiaji wa vyombo vingine vya usafiri ikiwemo pikipiki wameeleza adha wanayopitia pindi watumiapo barabara hiyo.
Mkuu wa kitengo cha matengenezo kutoka wakala wa barabara nchini (TANROADS) mkoa wa Geita Mhandisi Fredrick Mande akizungumza kwa njia ya simu amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa ofisi yake ina taarifa hiyo tayari na kwamba mkandarasi ameshasaini mkataba ili kuanza kazi ya kuziba mashimo hayo.