Wadau Geita wapongeza mfumo mpya wa NECTA
26 August 2024, 3:02 pm
Wanafunzi wa darasa la 7 kote nchini wanatarajia kuanza kufanya mtihani wa taifa wa kuhitimu elimu hiyo septemba 11 na 12 mwaka huu.
Na: Ester Mabula – Geita
Mkurugenzi wa shule ya awali na msingi Kadama Bi. Leticia Pastory amesema kuwa mabadiliko ya mfumo wa mtihani ya taifa kwa shule za msingi yanatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wanafunzi sambamba na kuondoa vitendo vya udanganyifu.
Ametoa kauli hiyo Agosti 23, 2024 katika mahafali ya kumi na nne ya shule ya msingi ya Kadama ambapo ameeleza kuwa mfumo mpya utaimarisha ubora wa elimu na kuwaandaa wanafunzi vizuri huku pia ukilenga kuwawezesha wanafunzi kuwa na uwezo wa kujieleza zaidi.
Katika hatua nyingine ameeleza maandalizi ya wanafunzi kuelekea mtihani huo ambapo amebainisha kuwa wamejiandaa vya kutosha na kwamba wanatarajia matokeo mazuri zaidi.
Mgeni rasmi kwenye mahafali hayo, Mboje Kisusi, amewasisitiza wazazi na walezi umuhimu wa kuwafundisha watoto wao maadili mema na kumjua Mungu, akiongeza kuwa elimu bora inapaswa kuendana na malezi bora.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na wazazi, walezi, na wadau mbalimbali wa elimu, ambapo walipongeza juhudi za shule hiyo katika kutoa elimu bora na kulea watoto vyema kimaadili, kitaaluma na kiroho kwa dini zote mbili.