Wadau wa kilimo wahimizwa kufanya tafiti zenye tija Geita
2 August 2024, 2:20 am
Dhana potofu kwa wakulima juu ya mbolea za viwandani imeendelea kukosesha wakulima fursa mbalimbali ikiwemo kupata mavuno mengi.
Na: Evance Mlyakado – Geita
Wadau wa kilimo mkoani Geita wametakiwa kufanya tafiti zenye kuleta tija ili kuwasaidia wakulima kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo kwa wakulima ili waweze kupata manufaa katika kilimo chao kwa maendeleo yao na nchi kwa ujumla.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela ambaye alipaswa kuwa mgeni rasmi katika kikao cha kupokea taarifa ya maendeleo ya sekta ya kilimo mkoa wa Geita kwa mwaka 2023/2024 na maandalizi ya msimo wa kilimo msimu wa 2024/2025 kilichofanyika Julai 31, 2024 mkuu wa wilaya ya Geita Hashimu A Komba amesema matumizi ya mbegu na mbolea katika maeneo sahihi kwa wakulima bado ni changamoto hivyo akawataka wataalamu wa kilimo kuwafikia wakulima katika maeneo yao.
Mkuu wa idara ya sekta za uchumi na uzalishaji kutoka ofisi ya mkoa wa Geita Dkt. Elphace Msenya amewataka wakulima kuondokana na dhana potofu juu ya matumizi ya mbolea za viwandani kwani wakulima wengi wamekuwa wakiamini kuwa mbolea za viwandani huharibu rutuba.
Baadhi ya wakulima waliohudhuria katika kikao hicho wamesema imani hizo zinachangiwa na wataalamu wa kilimo kutokuwafikia katika maeneo yao kwa wakati ili kuwapa elimu Zaidi.
Katika kuhakikisha kuwa wakulima wanafanikiwa kuwa na kilimo chenye tija mamlaka ya hali ya hewa kanda ya ziwa imewataka wakulima kuzingatia taarifa mbalimbali zinazotolewa na mamlaka hiyo kuhusu muenendo wa hali ya hewa katika maeneo yao
Nao baadhi ya wadau wa kilimo walioshiriki katika kikao hicho wameeleza kuwa wataendelea kutoa ushirikiano ikiwemo kuleta wataalamu wa kilimo ili kuendeleza kukuza sekta ya kilimo.