Mtendaji akataliwa baada ya kususia kikao cha kata
3 May 2021, 6:56 pm
Na Mrisho Sadick:
Kikao cha maendeleo ya kata katika kata ya Mganza wilayani Chato mkoani Geita kimeadhimia kwa pamoja kutofanya kazi na Afisa mtendaji wa kata hiyo baada ya kuonesha utovu wa nidhamu kwa kususia kikao hicho.
Inaelezwa kuwa sababu za afisa Mtendaji huyo kususia kikao hicho nipale alipoona waandishi wa habari ndani ya ukumbi wa mkutano waliyokuwa wamealikwa na diwani wa kata hiyo ndipo alipoamua kuondoka yeye pamoja na watendaji wengine wa serikali wa kata hiyo.
Baada ya afisa huyo kuondoka wajumbe wa mkutano huo wakiongozwa na Diwani wa kata ya Mganza Bw.Emannueli Mwita wamesema hawako tayari kufanya kazi na afisa huyo kwa kuwa ameamua kuwaondoa watumishi wote waserikali waliokua ndani ya kikao hicho na kuondoka nao ofisini kwake.
Wamesema kikao hicho ni cha wazi hivyo sababu ya mtendaji huyo kutotaka wandishi wa habari ndani ya kikao hicho ni kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari na kuwanyima haki wananchi ya kufahamu kile kinachofanywa na viongozi wao kwa maslahi ya umma.
Akizungumza kwa njia ya simu na Storm FM Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Chato Bw Eliud Mwaiteleke amesema siyo kila mtu anaweza kuwa msemaji wa taasisi nakutoa wito kwa waandishi wa habari kabla ya kuingia nakufanya kazi katika eneo hilo nivyema wakafika ofisini kwake ili kuondokana na changamoto kama hizo.