Wanafunzi darasa la nne zaidi ya 1,000 wamefeli Nyang’hwale
17 January 2024, 11:18 am
Kutokana na matokeo mabaya ya darasa la nne na kidato cha pili mwaka jana wilaya ya Nyang’hwale imeanza mikakati ya mapema ili kuepukana na changamoto hiyo mwaka huu.
Na Mrisho Sadick :
Kufuatia anguko la kufeli wanafunzi wa darasa la nne zaidi ya elfu moja 1,000 wilayani Nyang’hwale Mkoani Geita Mkuu wa wilaya hiyo Grace Kingalame ameapa kuwashughulikia walimu na watendaji wa idara ya elimu wanaoishindwa kutimiza majukumu yao kwa mujibu wa sheria wilayani humo.
Kingalame ametoa kauli hiyo kwenye Kikao cha tathimini na mipango ya Elimu kwa mwaka 2024 kufuatia matokeo mabaya ya Mtihani wa darasa la nne na kidato cha pili huku akisema atakuwa katili kwa watendaji wa serikali watakao kuwa kikwazo katika utekelezaji wa mkakati waliyojiwekea wa kuhakikisha wanakabiliana na changamoto zote zilizochangia matokeo mabaya huku akiagiza wanafunzi wote waliyofeli kuhakikisha wanafuatiliwa nakurudishwa shuleni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Husna Tony ameahidi kufanyia kazi changamoto zote zilizowasilishwa na wadau wa elimu zikiwemo za walimu kutotimiza wajibu wao ipasavyo, baadhi ya wazazi kuwashinikiza watoto kufanya vibaya na Utoro sugu.