Storm FM
Storm FM
12/03/2026, 18:33

Maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe ya Kijijini (SALIKI) hufanyika katika ngazi ya jamii kwa lengo la kuwaleta wananchi karibu na huduma muhimu za afya na lishe ili kujenga jamii yenye afya bora.
Na: Ester Mabula
Maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe ya Kijiji (SALIKI) yamefanyika leo Machi 12, 2026 katika mtaa wa Katoma, kata ya Kalangalala, yakihusisha utoaji wa huduma mbalimbali za afya kwa wananchi.
Huduma zilizotolewa wakati wa maadhimisho hayo ni pamoja na upimaji wa hali ya lishe, utoaji wa elimu ya lishe, huduma za chanjo, upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza pamoja na uchangiaji wa damu salama.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Diwani wa kata ya Kalangalala Reuben Sagayika, amwahimiza wazazi na walezi kuendelea kushiriki kikamilifu katika uchangiaji wa chakula shuleni ili kusaidia kuboresha afya na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi shuleni.

Aidha Diwani Sagayika amewakumbusha wanawake umuhimu wa kuhudhuria kliniki mara kwa mara wanapokuwa wajawazito ili kulinda afya zao na za watoto wanaotarajiwa kuzaliwa.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mganga mkuu wa manispaa ya Geita Dkt. Sunday Mwakyusa amesema mpango wa SALIKI ni sehemu ya utekelezaji wa kipengele kilichopo katika mkataba wa lishe unaotekelezwa kuanzia ngazi ya eneo hadi kitaifa huku akibainisha lengo la maadhimisho kuwa ni pamoja na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya lishe, kuhamasisha matumizi ya huduma za afya pamoja na kuboresha hali ya lishe kwa wananchi.
