Storm FM
Storm FM
06/03/2026, 23:06

Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya wanawake kwa mwaka huu ni “Haki na Usawa kwa wanawake na wasichana: Msingi wa maendeleo Jumuishi kufikia Dira ya 2050”.
Na: Ester Mabula
Wanawake 28 mkoani Geita wamepatiwa mitaji ya kuendeleza biashara zao na Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini Mhandisi Chacha Wambura.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Marchi 06, 2026 katika ukumbi wa Gedeco uliopo manispaa ya Geita mkoani Geita kwenye kongamano la wanawake lililoandaliwa na Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Geita kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani.
Awali kabla ya kukabidhi mitaji hiyo Mbunge wa Geita mjini Mhe. Chacha Wambura ambaye alikuwa mgeni rasmi amewataka wanawake kuondoa dhana ya utegemezi na badala yake wajihusishe katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Naye Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Geita Regina Mikenze amesema kwa sasa Rais Samia Suluhu ametoa mikopo kwa wanawake kwa mtu mmoja mmoja na kuwaomba wanawake wachangamkie fursa hiyo ili wajikwamue kiuchumi

Aizungumza Afisa maendeleo ya Jamii mkoa wa Geita Bi. Martha Kaloso amewaomba wanawake kujitokeza kwa wingi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Marchi 08, 2026 ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Geita.
Wakizungumza baadhi ya wanawake waliopatiwa mitaji hiyo Bi. Aziza Hassan na Suzana Thomas wamemshukuru Mbunge kwa kuwawezesha mitaji huku wakiahidi kuitumia kwaajili ya kuendeleza biashara zao.