Storm FM
Storm FM
23 February 2026, 9:20 am

Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetoa mchango wa shilingi milioni 50 kudhamini hafla ya Tanzania Water Service Excellence Awards inayofanyika jijini Arusha tarehe 23 Februari 2026.
Na: Ester Mabula
Tuzo hizo ni sehemu ya mkutano wa kitaifa wa mabaraza ya wakurugenzi wa mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira (WSSAs), unaoandaliwa na wizara ya maji kuanzia leo Februari 23 hadi 25, 2026 katika Hoteli ya Ngurudoto jijini Arusha.
Zaidi ya washiriki 1,000 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wenye lengo la kuimarisha uongozi, uwajibikaji na usimamizi bora katika mamlaka zinazohusika na utoaji huduma za maji nchini.
Akizungumza kuelekea hafla hiyo, Makamu wa Rais wa Masauala ya Uendelevu na Mahusiano ya Kampuni Afrika wa AngloGold Ashanti, Simon Shayo, amesema kuwa udhamini huo unaakisi dhamira ya muda mrefu ya kampuni katika kuchangia maendeleo endelevu na usimamizi makini wa rasilimali.

“Maji ni rasilimali muhimu kwa ukuaji wa uchumi, maendeleo ya viwanda na ustawi wa jamii. Usimamizi bora wa rasilimali hii una athari ya moja kwa moja kwa uimara wa biashara na maendeleo ya taifa kwa ujumla. Kwa kuunga mkono tuzo hizi, tunasisitiza umuhimu wa kuimarisha uongozi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za maji ili kulinda mustakabali wa kiuchumi na kijamii wan chi yetu” alisema Shayo.
Kwa miaka iliyopita, GGML imetekeleza miradi ya maji mkoani Geita, ikiwemo kuchangia mradi wa maji wa Geita uliowezesha zaidi ya wananchi 300,000 kupata huduma ya maji safi na salama pamoja na kuboresha miundombinu ya usambazaji wa maji katika maeneo yanayozunguka mgodi.
Naye Dkt. Kiva Mvungi, Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama na Mazingira wa GGML, alibainisha kuwa usimamizi endelevu wa maji ni sehemu muhimu ya mikakati ya uendeshaji wa kampuni na mchango wake kwa jamii.
Upatikanaji wa maji safi na salama unaendelea kuwa kipaumbele katika ajenda ya maendeleo ya Tanzania. Kupitia udhamini huu, GGML inaungana na juhudi za kitaifa za kuboresha viwango vya utoaji huduma na kutambua ubunifu katika sekta ya maji, kwa lengo la kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora na endelevu.
