Storm FM
Storm FM
18 February 2026, 12:56 pm

Jumla ya wanafunzi 65 waliohitimu kidato cha nne katika shule ya sekondari ya wavulana ya Geita walipata ufaulu wa daraja la kwanza (division one).
Na: Ester Mabula
Walimu wa shule ya sekondari ya wavulana ya Geita (GESECO) wamepewa tuzo kufuatia ufaulu mzuri wa daraja la kwanza (division 1) kwa wanafunzi 65 wa kidato cha nne waliohitimu mwaka 2025.
Hafla ya pongezi imefanyika Februari 17, 2026 shuleni hapo na kuhudhuriwa na wanafunzi, walimu, wazazi pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali ambapo zawadi mbalimbali zimetolewa ikiwemo pikipiki pamoja na fedha kwa viwango tofauti tofauti.
Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Makamu mkuu wa shule Mwl. Venance Mushi amesema shule hiyo inakabiliwa na uchakavu wa miundombinu sambamba na ukosefu wa uzio hali inayopelekea usumbufu kwa wanafunzi.

Mgeni rasmi, Diwani wa kata ya kalangalala Reuben Sagayika kwa niaba ya Mstahiki meya wa manispaa ya Geita amewapongeza walimu kwa kazi kubwa na nzuri huku akiwasilisha zawadi kutoka halmashauri ya manispaa ya Geita kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri.
Kuhusu changamoto ya miundombinu, Mgeni rasmi ameahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 2 huku akiahidi kukusanya fedha na vitendea kazi kutoka kwa wadu ili kukarabati uzio wa shule hiyo.

Katika hatua nyingine ofisi ya mbunge Jimbo la Geita mjini imetoa kiasi cha shilingi laki 5 kwa mkuu wa shule pamoja na shilingi laki 3 kila mmoja kwa walimu wa masomo yaliyofanya vizuri ambayo ilikabidhiwa na Katibu wa Mbunge Rizick Marko.

Awali akiwasilisha salamu za mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Afisa elimu taaluma sekondari Singo Jumaamesema ofisi ya mkurugenzi wa manispaa inatarajia kuandaa hafla kubwa ya kuwapongeza walimu wa shule za sekondari waliofanya vizuri kwenye matokeo.
