Storm FM
Storm FM
15 February 2026, 11:38 am

“Nataka niseme kuanzia siku ya Jumanne, barabara zitaanza kufanyiwa matengenezo ili basi kero hii iweze kuondoka kwa wananchi wa eneo hili kwani serikali ya Rais Samia imetupa fedha kwaajili ya kukarabati miundombinu” – Mbunge Chacha Wambura
Na: Ester Mabula
Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini Mhandisi Chacha Wambura amefanya ziara ya kukagua miundombinu ya elimu pamoja na barabara katika kata ya Buhalahala, ikiwa ni sehemu ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero za wananchi.
Katika ziara hiyo aliyoifanya Februari 14, 2026 ametembelea mitaa ya Kambarage, Michungwani na Nshinde ambapo awali aliweza kusikiliza kero za wananchi ambao wameeleza juu ya changamoto ya miundombinu ya barabara wakieleza kuwa wakati wa mvua barabara hizo hupitika kwa shida, hali inayochelewesha huduma za kijamii na kuathiri biashara.

Mbunge Chacha ameahidi kutatua kero hiyo ya miundombinu ya barabara katika maeneo aliyotembelea akisema zoezi la ukarabati litaanza Jumanne ya Februari 17, mwaka huu huku diwani wa kata ya Buhalahala Doto Nzanzui akimpongeza kwa kutenga muda wake na kuwafikia wananchi ili kukatua kero zao
Katika ziara hiyo, Mbunge Chacha aliambatana na mhandisi Jerry Mwakapemba kutoka ofisi ya TARURA wilaya ya Geita ambaye alitoa maelezo kuhusu mpango wa ukarabati wa barabara hizo.
