Storm FM
Storm FM
26 January 2026, 6:04 pm

Ugawaji wa hati za kimila ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wanakuwa na umiliki halali wa ardhi.
Na Mrisho Sadick:
Kuelekea siku 100 za uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakulima na wafugaji wa vijiji viwili katika Wilaya ya Nyang’hwale, mkoani Geita, wameishukuru Serikali kwa kutatua changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa maeneo ya malisho na kilimo.
Wananchi hao wamekabidhiwa maeneo ya ardhi pamoja na hati za kimila 838, hatua iliyowezekana baada ya Serikali kumega ekari 3,101 kutoka Msitu wa Hifadhi wa Miyenze kwa matumizi ya wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Bi. Grace Kingalame, ameongoza zoezi la ugawaji wa hati hizo ambapo kijiji cha Bujulamiyenze kimepata hati 541 huku kijiji cha Ihushi kikikabidhiwa hati 297.

Wanufaika wa hati hizo wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa haraka wa zoezi hilo, wakisema limefanyika kabla ya kutimia siku 100 za uongozi wake, jambo linaloonesha dhamira ya Serikali katika kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Akizungumza katika zoezi hilo, Mkurugenzi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Usimamizi na Uratibu kutoka Timu ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Bw. Jonas Masingija, amesema ugawaji wa hati za kimila ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wanakuwa na umiliki halali wa ardhi ili kuepusha migogoro na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.