Storm FM
Storm FM
19 January 2026, 6:39 pm

Kundi la watu wenye ulemavu linaendelea kukumbana na changamoto mbalimbali, hususan wanawake wanaotelekezwa.
Na Mrisho Sadick:
Mwanamke mwenye ulemavu Sarah Malale mkazi wa Kata ya Lulembela Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita amewaomba Watanzania wenye mapenzi mema kujitokeza kumsaidia baada ya kutelekezwa na mume wake na kubaki na jukumu la kuwahudumia na kuwatunza watoto wake wanne peke yake.
Ni simulizi yenye maumivu lakini pia tumaini kwa Bi. Sarah, ambaye tangu aachwe na mume wake amekuwa akiishi katika mazingira magumu ya maisha, anasema hana kipato cha uhakika cha kuendeshea familia yake, huku makazi anayoishi kwa sasa akiwa amepatiwa kwa muda tu na msamaria mwema.

Akizungumza kwa tabasamu licha ya changamoto kubwa anazokabiliana nazo, wakati Shirika la Mtetezi wa Mama Mkoa wa Geita lilipofika nyumbani kwake kumpatia msaada wa kibinadamu Bi. Sarah ameeleza hali halisi ya maisha yake na mahitaji ya msingi anayokosa yeye pamoja na watoto wake.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Geita Paul Malimi amesema kundi la watu wenye ulemavu linaendelea kukumbana na changamoto mbalimbali, hususan wanawake wanaotelekezwa, na kuomba jamii kutoa ushirikiano wa karibu ili kuendelea kukabiliana na changamoto hizo.
Naye Afisa Maendeleo wa Kata ya Lulembela Catty Neata amebainisha kuwa ofisi yake itaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya familia hiyo, huku akiwasihi wadau na mashirika yasiyo ya kiserikali kujitokeza kusaidia makundi yenye uhitaji mkubwa katika jamii.
Kwa upande wao viongozi wa Shirika la Mtetezi wa Mama wamesema wameguswa na hali ya familia ya Bi. Sarah, na kuahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mwanamke huyo na watoto wake wanapata msaada wa kudumu na stahiki.