Storm FM
Storm FM
16 January 2026, 7:16 pm

“Nina imani kuwa ugawaji wa hati za kimila utapunguza kwa kiasi kikubwa uwepo wa migogoro ya ardhi” -Katibu tawala mkoa wa Geita Mohamed Gombati
Na: Edga Rwenduru
Baada ya serikali kumega sehemu ya eneo la hifadhi ya msitu wa muyenze na kuwapatia wakazi wa vijiji cha Ihushi na Bujuramuyenzi vilivyopo wilayani Nyangh’wale mkoani Geita kwaajili ya makazi na kilimo, Tume ya mipango ya matumizi ya Ardhi imeanza mchakato wa upimaji wa ardhi hiyo kwaajili ya kutoa hati za kimila 1,200 kwa wakazi wa vijiji hivyo.
Akizungumza mara baada ya Tume hiyo kuwasili mkoani Geita, Katibu tawala wa mkoa wa Geita Mohamed Gombati amesema ugawaji wa hati za kimila utapunguza kwa kiasi kikubwa migogoro ya ardhi iliyokuwepo kutokana na wakazi wa vijiji hivyo kuvamia maeneo ya hifadhi ya Muyenze na kuanzisha makazi na kilimo kinyume na utaratibu.

Kwa upande wake John Chuwa msimamizi wa timu ya wataamu kutoka tume ya mipango ya matumizi ya Ardhi amesema zoezi la upimaji maeneo hayo kwaajili ya kutoa hati za kimili katika vijiji hivyo viwili utadumu kwa muda wa siku 14.

Kaimu kamishina msaidizi wa Ardhi mkoa wa Geita Oscar Yohana ametoa wito kwa viongozi wa serikali za mitaa kuhamasisha wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa tume watakapofika kwenye maeneo yao kwaajili ya kufanya upimaji wa ardhi.
