Storm FM
Storm FM
13 January 2026, 11:31 am

“Wanawake watatumaliza, kwanini mtu asieleze kuwa kaolewa ili kuondoa matatizo yasiyo ya lazima” – Kijana aliyefumaniwa
Na: Ester Mabula
Kijana mmoja (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka 34 amenusurika kifo baada ya kushambuliwa na wananchi wenye hasira kali, baada ya kufumwa akiwa na mke wa mtu chumbani katika eneo la Bujora, Kata ya Mission, wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Akizungumzia tukio hilo Januari 12, 2026, kijana huyo akiwa chini ya ulinzi wa polisi jamii amedai kuwa mwanamke huyo alimdanganya kuwa hajaolewa ambapo ndipo alianzisha nae mahusiano.
Mwanamke aliyekamatwa ugoni na kijana huyo (jina limehifadhiwa) amesema kuwa kilichopelekea hayo ni kutokana na mume wake kushindwa kuihudumia na kuitunza familia .
Akizungumzia tukio hilo, mume wa mwanamke huyo (jina limehifadhiwa) amedai kuwa hajawahi kuitelekeza familia yake na wala hana mke mwingine kama inavyoelezwa.
Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya wakazi wa mtaa huo wamesikitishwa na tukio hilo na kuwaomba wanawake kuwa waaminifu kwenye ndoa zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mtaa wa Mission Bw. Joseph Protas amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuitaka jamii kuachana na vitendo hivyo ili kuepuka kuhatarisha maisha yao kwani baadhi ya wananchi kujawa jazba na kujichukulia sheria mkononi.